Sunday, 25 December 2011
Mashairi: Siku Macho Nikifumba (Sisitizo)
Twaha H. M Kiobya [Mujaahid]
TIOT Morogoro
1. Bismillah naanza, kwa jina la utukufu
Nia watu kuwafunza, Natumia hii safu
Niepushe ya kuponza, wafanye uadilifu
Hayatasaidia wafu, Masadaka ya matanga
2. Uloyatenda mwenyewe, kabla ya kutawafu
Mazuri au yasiwe, atakulipa Raufu
Hata kama usomewe, mahitaji maradufu
Hayatasaidia wafu, ma-sadaka ya matanga
3. Wale nyama au sunga, hayafuti ulanifu
Hawawezi pata mwanga, wale washibe wakinifu
Haya ninyi mwajivunga, tatu hazifiki wafu
Hayatasaidia wafu, ma-sadaka ya matanga
4. Ni uzushi kwenye dini, hajasema Ashrafu
Si kitu arobaini, utapooza minofu
Wale wakudanganyeni, ma vyakula na sarafu
Hayatasaidia wafu, ma-sadaka ya matanga
5. Msimbe hayo yashike, mshairi maarufu
Kwenye uzushi utoke, ufate wasadikifu
Usingoje uumbuke, ya uzushi ni uchafu
Hayatasaidia wafu, ma-sadaka ya matanga
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment