Sunday, 25 December 2011
Tofauti Baina Ya Mwanamume Na Mwanamke Katika Uislamu
Tabia na Maumbile:
Mwanamme ameumbwa kutokana na udongo/tope/vumbi na mwanamke kaumbwa kwa ubavu.
Allaah Amekadiria ada [hedhi] ya mwezi kwa mwanamke na sio kwa mwanamme.
Mwanamme huota ndevu lakini mwanamke haoti, na ikiwa ataota basi anaruhusiwa kuzinyoa.
Wanawake ni wapungufu wa ibada na uwezo wa kufikiri. Mathalan katika utoaji wa ushahidi, mwanamme mmoja ni sawa na wanawake wawili. Vile vile wakati wa ada zao za mwezi [hedhi] huwa hawafungi wala kuswali.
Wanaume wamepewa madaraka juu ya kuwasimamia wanawake.
Manii ya mwanamme ni meupe na ya mwanamke ni manjano.
Ni wajib kufanyiwa tohara [jando] kwa mwanamme na ni Sunnah kwa mwanamke.
Kutoga masikio kwa ajili ya mapambo kumeruhusiwa kwa wanawake na sio kwa wanaume.
Twahara:
Mkojo wa mwanamke una harufu kali na najsi zaidi kuliko wa mwanamme.
Inapendekezeka kwa mwanamme kutia wudhuu tena pindi anapotaka kurejea pahali pale pale katika tendo la jimai.
Swalaah:
Adhana na Iqaamah sio lazima kwa wanawake na sio sawa kwa mwanamke kuadhini.
Mwanamke huswali nyuma ya mwanamme, hata ikiwa mwanamke huyo yupo peke yake. Lakini mwanamme Swalaah yake itakuwa si sawa (haipendezi) ikiwa ataswali peke yake nyuma ya mwanamme mwenziwe.
Mwanamke hawezi kuwa Imaam wa wanaume kwenye Swalaah.
Ikiwa mwanamke anawaswalisha wanawake wengine, ni lazima asimame katikati ya safu. Wakati mwanamme aposwalisha husimama mbele peke yake.
Swalaah ya Jama’ah ni waajib kwa wanaume na sio kwa wanawake.
Safu iliyo bora kwa mwanamke katika Swalaah ya Jama’ah ni safu ya nyuma, na iliyo bora kwa mwanamme ni safu ya mwanzo.
Imependekezwa kwenda kuswali Msikitini Swalaah za usiku kwa wanaume na sio kwa wanawake.
Ikiwa Imaam atakosea katika Swalaah, mwanamke anatakiwa kupiga kofi lakini mwanamme hutakiwa kusema “Subhaana-Allaah”
Wanawake hawalazimiki kuhudhuria Swalaah ya Ijumaa, wanaume ni lazima.
Wanawake hawatoi khutbah ya ‘Iyd, Ijumaa, kupatwa kwa jua au mwezi, wala Swalaah ya kuomba mvua.
Swalaah hukatika ikiwa mwanamke atapita mbele ya mwanamme anayeswali, na ikiwa mwanamme atapita mbele ya mwanamme anayeswali basi Swalaah yake huwa ni sahihi.
Swalaah ya ‘Iyd ni waajib kwa wanaume, lakini si kwa wanawake. Hata hivyo imependekezwa kwa wanawake kuhudhuria ikiwa kutakuwa hakuna jambo litakaloleta fitna.
Swalaah ya Maiti:
Jama’ah husimama upande wa kichwani ikiwa wanamswalia maiti wa kiume na husimama katikati ikiwa ni maiti mwanamke.
Haipendezi kwa wanawake kuzuru makaburini, lakini wanaume wameshauriwa kufanya hivyo.
Wanawake hawawezi kusindikiza msafara wa mazishi, lakini wanaume wanaweza.
Wanawake wanapokufa huoshana na kuvishana sanda wao kwa wao, na wanaume pia ni hivyo hivyo isipokuwa ikiwa ni mume na mke.
Zakaah na Swadaqah:
Wanawake wamehimizwa kutoa Swadaqah zaidi kuliko wanaume
Mwanamke anaweza kuwapa Zakaah watoto wake na mumewe, lakini mwanamme hawezi kuwapa Zakaah watoto wake wala mkewe.
Fidia ni jukumu lake mwanamme na sio mwanamke. Hii hutokea ikiwa mwanamme kwa makusudi kafanya kitendo cha ndoa na mkewe katika mchana wa mwezi wa Ramadhaan.
Mwanamke hawezi kufunga Swawm za Sunnah bila ya ruhusa ya mumewe. Mwanamme anaweza kufunga Swawm za Sunnah bila ya ruhusa ya mkewe.
Hijjah:
Mwanamke ni lazima awe na mtu asiye weza kumuoa (Mahram) wakati wa safari.
Mwanamke hatakiwi kunyanyua sauti yake wakati wa Talbiyah, mwanamme anatakiwa anyayue sauti yake.
Ihraam ya mwanamke ni zile zile nguo zake za safari sio lazima nyeupe.
Mwanamme anaweza kufanya Ramal, yaani kwenda mbio ndogo ndogo baina ya Swafaa na Marwaa, na kuizunguka Ka’bah; mwanamke hatakiwi kufanya hivyo.
Haishauriwi kwa wanawake kujaribu kubusu au kugusa Jiwe Jeusi wakati wa msongamano.
Mwanamme anaweza kupanda kilima cha Swafaa na Marwaa, mwanamke hatakiwi kufanya hivyo.
‘Aqiyqah
Mtoto wa kiume huchinjiwa kondoo wawili, mtoto wa kike huchinjiwa kondoo mmoja.
Jihaad, Vita, na Uongozi
Hakuna wanawake waliokuwa Manabii wala Mitume.
Mwanamke hawezi kuwa kiongozi wa watu wala jeshi.
Mtume (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifungamana agano kutoka kwa wanaume kwa kupewa mkono wa bay’ah na kaungwa mkono na wa wanawake kupitia matamshi.
Si kama ilivyo kwa wanaume, Wanawake hawawajibiki kupigana Jihaad. Hata hivyo kuna baadhi ya hali ambazo ni lazima ziambatanishwe kabla wanaume hawajajiingiza katika wajibu huu.
Ndoa, Talaka, na Eda:
Wanawake wanapewa talaka, sio wanaume.
Wanaume wana mamlaka ya talaka, ndoa na kutoa mahari; sio wanawake.
Mwanamme anaweza kuoa mwanamke wa Ahlul-Kitaab [Mayahudi na Wakristo] ikiwa mwanamke huyo sio mzinifu. Mwanamke hana haki hii ya kuolewa na mwanamme wa Ahlul-kitaab.
Mwanamme anaweza kuowa mke zaidi ya mmoja. Mwanamke hawezi kuwa na mume zaidi ya mmoja.
Harusi na karamu ya harusi (walima) ni jukumu la mwanamme na sio mwanamke.
Imeruhusiwa kwa wanawake kupiga dufu katika harusi zao. Hii hairuhusiwi kwa wanaume.
Matengenezo, na majukumu na huduma za familia ni jukumu la wanaume na sio wanawake.
Mwanamke yupo chini ya mamlaka ya mumewe. Mwanamme hayupo chini ya mamlaka ya mkewe.
Mwanamke hawezi kutembelewa katika nyumba na mtu yoyote bila ya kupata ruhusa ya mumewe. Mwanamme hahitajii ruhusa kutoka kwa mkewe.
Malaika humlaani mwanamke ikiwa atamtenga mume wake katika kitanda. Mwanamme hapati laana ikiwa atafanya hivyo.
Mwanamke ni lazima apate ruhusa ya mumewe kabla hajatoka nyumbani. Mwanamme hahitajii ruhusa ya mkewe anapotoka nyumbani.
Mwanamme hana eda isipokuwa anapotaka kumuoa dada au mama mdogo wa mke aliyemuacha. Hata hivyo ikiwa mwanamme atamuacha mkewe wa nne na akataka kumuoa tena basi itambidi amsubiri mpaka amalize eda yake.
Mavazi na Mapambo:
Mwanamke ameshauriwa kujipamba akiwa ndani ya nyumba yake na kwa ajili ya mume wake.
Ni haramu kwa mwanamke kujishabihisha na wanaume kwa mavazi yao. Na mwanamume pia haipasi kujishabihisha na wanawake.
Ni wajibu kwa wanawake kurefusha nguo zao zivuke chini ya vifundo vya miguu yao. Mwanamme kurefusha suruali na kanzu hadi zikavuka chini ya mafundo ya miguu ni haramu.
Mwanamke hatakiwi abadilishe nguo zake isipokuwa akiwa yumo ndani ya nyumba yake au pahali pa stara. Haya hayapo kwa wanaume.
Hijabu ya mwanamke ni lazima afunike mwili wote na uso.
Wanawake wameruhusiwa kuvaa mapambo ila tu asiyadhihirishe kwa wasio mahaarim wake.
Wanaume hawawezi kuvaa hariri, lakini wanawake wanaweza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment