Sunday, 25 December 2011
Umuhimu Wa Kutoa Zakaah Na Malengo Yake
Baada ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu Wata’ala) na kisha kumtakia rehma Mtume wake (Salla Allaahu ‘Alayhi Wasallam) tunawaletea somo la Zakaah kwa muhtasari hasa katika baadhi ya vipengele muhimu ambavyo vinatugusa katika jamii yetu.
Somo hili limekuja baada ya kufanya utafiti mdogo tu katika mwaka 2004 hapa Uingereza kwa jamii ya Waislamu wanaozungumza Kiswahili ili kujua kama wanaitekeleza nguzo hii au vinginevyo.
Mojawapo katika masuala yaliyokuwemo kwenye kidadisi ni kama mhusika ana elimu ya aina yoyote kuhusu Zakaah. Katika watu 75 waliojaza ni 26 tu waliokuwa wanaifahamu Zakaah na waliobaki hawakuwa na elimu ya kutosha kuhusu nguzo hii.
Pia watu 65 walikubali kwamba wanaweza kuwa na sifa za kuweza kutoa Zakaah na ni 10 waliosema hawana sifa hizo. Na katika 65 waliokubali ni 25 waliosema kwamba wanaitekeleza nguzo hii kikamilifu.
Katika sababu kadhaa zilizotajwa kwa Waislamu kushindwa kuitekeleza nguzo hii ni kuwa na imani dhaifu, uchoyo wa mali, kudhani kama kiwango kinachotolewa ni kikubwa, kuipenda dunia zaidi na kutozijua haki zake Allaah (Subhaanahu Wata’ala) na pia upatikanaji wenyewe wa mali kutingwa na utata.
Somo la Zakaah ni somo pana na lililosheheni elimu inayohitajika kwa kila mmoja wetu kulifahamu vyema ili aweze kuitekeleza nguzo hii kikamilifu kwani ni mojawapo katika nguzo tano za Kiislamu.
Somo hili pia lilifanyika katika Darsa za Ramadhaan 1428, Septemba - Oktoba 2007 katika mji wa Northampton – Uingereza.
Somo tumeligawa katika vifungu vifuatavyo kutokana na umuhimu wake na mazingira yaliyopo.
1. UMUHIMU WA KUTOA ZAKAAH NA MALENGO YAKE
2. MASHARTI YANAYOMUWAJIBIKIA MWENYE KUTOA ZAKAAH
3. ZAKAAH YA MAPAMBO YA DHAHABU
4. ZAKAAH YA FEDHA TASLIMU, BIDHAA NA MALI YA BIASHARA
5. KWA NINI MALI YA HARAMU HAITOLEWI ZAKAAH
Tumeonelea tuzungumzie vipengele hivi kwani vina nafasi kubwa katika maisha yetu ya kila siku na pia kutokana na masuala mengi yanayoulizwa kuhusu Zakaah yameonekana kuelemea zaidi katika vipengele hivi tulivyoviainisha. Na pia ni kutoa picha na hima kwa wanaotaka kuitekeleza nguzo hii kuwa na sehemu ya kuweza angalau kupata msingi wa taratibu za nguzo hii muhimu.
UTANGULIZI
Moja katika mipangilio ni kwamba kila kitu kilichopo ni Chake Allaah (Subhaanahu Wata’ala) na kumilikiwa na binadamu kama ni amana tu. Amana hii hukabidhiwa kwa muda tu na kwa masharti na jinsi Allaah (Subhaanahu Wata’ala) Anavyotaka. Na katika moja ya mipangilio yake (Subhaanahu Wata’ala) ni Zakaah.
Neno Zakaah katika lugha ya kiarabu lina maana ya tohara, baraka, kutakasa na pia kuongeza.
Kisheria ni kile kiwango cha mali ambacho Waislamu wanapaswa kukitoa ikiwa kama ni haki yake Allaah (Subhaanahu Wata’ala) na kuwapa wanaostahiki.
Ni nguzo ya tatu katika nguzo tano za Kiislamu na amri Yake Allaah (Subhaanahu Wata’ala) ambayo ni wajibu kutekelezwa na kila Muislamu mwenye uwezo. Zakaah si malipo, kodi, ada au takrima bali ni moja katika taasisi iliyoasisiwa na Allaah (Subhaanahu Wata’ala) ili kuleta uwiano katika neema Alizowajaalia waja wake.
Zakaah ilifaradhishwa katika mwaka wa pili wa Kiislamu – Hijriyah kwa mujibu wa kauli yenye nguvu.
Dalili za kufaradhiswa kwake ni aya zifuatazo katika Qur-aan:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا
Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwazo [At-Tawbah: 10]
Vilevile:
وَالَّذِينَ فِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ مَّعْلُومٌ
لِّلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ
Na ambao katika mali yao iko haki maalumu
Kwa mwenye kuomba na anayejizuilia kuomba. [Al-Ma’arij 24-25]
Na katika Sunnah:
قال صلى اللّه عليه وسلم لمعاذ حين أرسله إلى اليمن: (أعْلِمْهُم أن اللّه افترض عليهم في أموالهم صدقة
تؤخذ من أغنيائهم وترد على فقرائهم.) أخرجه الجماعة.
Amesema Mtume (Salla Allaahu ‘Alayhi Wasallam) kumwambia Mu’aadh pale alipomtuma Yemen: “Wafundishe kwamba Allaah Amewafaradhishia katika mali zao sadaka (Zakaah) huchukuliwa kutoka matajiri miongoni mwao na kurudishwa kwa mafakiri” Imetolewa na Jamaa
Zakaah na Sadaka ni maneno mawili ambayo humaanisha kitu kimoja kama ilivyokuwa katika Qur-aan na katika Sunnah za Mtume (Salla Allaahu ‘Alayhi Wasallam). Na pia wakati mwengine hutumika katika sura mbili ikiwa Zakaah ni Wajibu na sadaka ni isiyokuwa wajibu.
UMUHIMU WA KUTOA ZAKAAH
1. Inawakumbusha Waislamu kwamba kila walichojaaliwa ni neema kutoka kwake (Subhaanahu Wata’ala) na Allaah Hupenda neema zake kutumika jinsi alivyoagiza.
2. Mwenye kutoa Zakaah hutekeleza ibadah na mojawapo katika nguzo kuu za Kiislamu. Ibadah ambayo kila Muislamu mwenye uwezo huwajibika nayo kuitekeleza.
3. Mwenye kupewa Zakaah hupewa ikiwa ni kama moja ya shukrani Zake Allaah (Subhaanahu Wata’ala) na miongoni mwa haki zake.
4. Wenye kutoa Zakaah ndio waliojaaliwa sifa ya waumini wa kweli kwa mujibu wa Qur-aan
إِنَّمَا يَعْمُرُ مَسَاجِدَ اللّهِ مَنْ آمَنَ بِاللّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ وَأَقَامَ الصَّلاَةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَلَمْ يَخْشَ إِلاَّ اللّهَ فَعَسَى أُوْلَـئِكَ أَن يَكُونُواْ مِنَ الْمُهْتَدِينَ
Wanaoamrisha misikiti ya Allaah ni wale wanaomuamini Allaah na siku ya mwisho na kusimamisha Sala na kutoa Zakaah na hawamuogopi yeyote isipokuwa Allaah basi hao ndio wanaotarajiwa kuwa miongoni mwa waliooongoka. [at-Tawbah: 18]
ZAKAAH HUMSAIDIA MUISLAMU KATIKA MAISHA YA KIDUNIA
Kwa:
1. Kupata radhi Zake Allaah (Subhaanahu Wata’ala).
لَن تَنَالُواْ الْبِرَّ حَتَّى تُنفِقُواْ مِمَّا تُحِبُّونَ وَمَا تُنفِقُواْ مِن شَيْءٍ فَإِنَّ اللّهَ بِهِ عَلِيمٌ
Hamtoweza kuufikia wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda. Na chochote mtakachokitoa basi hakika Allaah anakijua. [Aali ‘Imraan: 92]
2. Kuzidisha baraka na kuongezeka kwa mali.
وَمَا آتَيْتُم مِّن رِّبًا لِّيَرْبُوَ فِي أَمْوَالِ النَّاسِ فَلَا يَرْبُو عِندَ اللَّهِ وَمَا آتَيْتُم مِّن زَكَاةٍ تُرِيدُونَ وَجْهَ اللَّهِ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الْمُضْعِفُونَ
Na mnachokitoa kwa riba ili kiongezeke katika mali ya watu, basi hakiongezeki mbele ya Allaah. Lakini mnachokitoa kwa Zakaah kwa kutaka radhi ya Allaah, basi hao ndio watakaozidishiwa. [Ar-Ruum: 39]
3. Kuzidisha mapenzi na kuenziana katika jamii na kuzidisha udugu halisi wa Kiislamu
وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاء بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلاَةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللّهَ وَرَسُولَهُ أُوْلَـئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللّهُ إِنَّ اللّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ
Na wanaoamini wanaume na wanaoamini wanawake ni marafiki wao kwa wao huyaamrisha yaliyo mema na huyakataza yaliyo mabaya na husimamisha Sala na hutoa Zakaah na humtii Allaah na Mtume wake. Hao ndio ambao Allaah Atawarehemu. Hakika Allaah ni Mwenye nguvu na Mwenye hekima. [At-Tawbah: 71]
ZAKAAH HUMSAIDIA MUISLAMU KATIKA MAISHA YA AKHERA
1 Ni sababu ya kusamehewa madhambi yetu
إِن تُقْرِضُوا اللَّهَ قَرْضًا حَسَنًا يُضَاعِفْهُ لَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ وَاللَّهُ شَكُورٌ حَلِيمٌ
Na mkimkatia Allaah sehemu nzuri (katika mali zenu mkazitoa kwa njia ya kheri) Atakuzidishieni na Atakughufurieni. Na Allaah Ndiye mwingi wa Shukrani na mpole. [At-Taghaabun-17]
2 Ni sababu ya kutakaswa na kusamehewa madhambi
إِن تُبْدُواْ الصَّدَقَاتِ فَنِعِمَّا هِيَ وَإِن تُخْفُوهَا وَتُؤْتُوهَا الْفُقَرَاء فَهُوَ خَيْرٌ لُّكُمْ وَيُكَفِّرُ عَنكُم مِّن سَيِّئَاتِكُمْ وَاللّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ
Kama mkitoa sadaka kwa dhahiri ni vizuri na kama mkitoa kwa siri na kuwapa mafakiri basi huo ni ubora zaidi kwenu na atakuondoleeni maovu yenu na Allaah Anazo habari za mnayoyatenda. [Al-Baqarah: 71]
MALENGO YA KUFARADHISHWA KWAKE
Zakaah imefaradhishwa na Allaah (Subhaanahu Wata’ala) na ndani yake kuna malengo zaidi ya yale anayoyafahamu binadamu kwamba ni kwa ajili ya kuwasaidia maskini na wasiojiweza tu. Yafuatayo ni baadhi tu ya malengo yanayopatikana katika Zakaah kwa ufupi:
1 Humtoharisha Muislamu nafsi yake na kuondosha ubakhili katika mali kama ilivyoripotiwa kutoka kwa Shaykhul Islaam Ibnu Taymiyah (Allaah Amrehemu):
نفس المتصدق تزكو، وماله يزكو، يطهر ويزيد في المعنى
Nafsi ya mwenye kutoa Sadaka hutoharika na mali yake husafika na hutoharika na kuongezeka kimaana halisi.
2 Humuondoshea husda maskini na fakiri kwani ni khulka ya binadamu kuwa na choyo.
3 Huisafisha mali kwani haki iliyomo ndani yake haistahiki kubaki na mwenye mali si milki yake tena.
4 Huongeza baraka kwani kutoa Zakaah ni kutekeleza moja katika haki za mali. Ingawa mwenye kuitoa ataona kupungukiwa kwa mali kihali halisi lakini faida yake huwa ni baraka na neema.
عن أبي هريرة رضي الله عنه أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ما نقصت صدقة من مال، وما زاد الله عبدًا بعفوٍ إلا عزًّا، وما تواضع أحد لله إلا رفعه الله رواه مسلم
Kutoka kwa Abu Hurayrah Allaah (Amuwie radhi) amesema; Mtume (Salla Allaahu ‘Alayhi Wasallam) amesema: “Haitopungua mali kwa kutolewa sadaka na hamzidishii Allaah mja wake kwa kumnyima ila humfanya kuwa na nguvu na na yeyote mwenye kujidhalilisha kwa Allaah basi Allaah humnyanyua (daraja)” Muslim
5 Huondosha ufakiri katika jamii ikitekelezwa kikamilifu kwani tabaka la wasiojiweza hupungua na hatimae kutokomea.
6 Ni njia ya kujenga utamaduni wa kutoa kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu Wata’ala). Mwenye kuitekeleza nguzo hii humwia rahisi na kuwa na mazowea ya kutoa hasa katika amali nyengine za kheri.
7 Kuwapa mtihani waja wake kwani nafsi imeumbwa katika kupenda mali na utajiri hivyo kwa atakayekuwa tayari kutoa hufanya hivyo kwa ajili ya kutaka radhi Zake Allaah (Subhaanahu Wata’ala) na hivyo kuvuka mtihani huu mzito.
8 Hujenga jamii yenye kusaidiana na kujaliana kwani uislamu unakataza kuwepo jamii inayoomba omba au isiyojitosheleza. Hili ni jambo la kuzingatiwa kwa kila anaeishi chini ya kivuli cha Kiislamu kuhakikisha mwenye uwezo kumsaidia asiyekuwa na uwezo.
HEKIMA YA KUFARADHISHWA KWAKE
Ni wajibu kuzingatia kwamba Allaah (Subhaanahu Wata’ala) hafaradhishi kitu isipokuwa kuna maslahi na faida. Tunaweza kuyaona maslahi yake na pia tusiyafahamu. Ila tu ni wajibu kwetu kuitakidi kwamba kila Allaah (Subhaanahu Wata’ala) Alichokileta basi kuna hekima ndani yake. Huu ni mmoja katika misingi ya Aqiydah sahihi ya Muislamu.
Pia imethibitika kivitendo faida ya Zakaah ikitekelezwa kikamilifu enzi za Ukhalifa wa ‘Umar Ibnul ‘Abdil-‘Aziyz, (Allaah Amuwie radhi), ambapo iliweza kukusanywa na hakukuwepo maskini au mafakiri wa kupewa na iliishia Baytul Maal. Jamii iliweza kufikia hali ya maisha ambapo hakuna Waislamu waliokuwa wakihitaji Zakaah.
Maulamaa wamezielezea hekima nyingi sana kama zifuatazo:
1 Kukamilika Uislamu wa mja
Zakaah ni mojawapo ya nguzo za Kiislamu. Kuitekeleza ni kukamilisha mihimili mikuu ya dini yetu. Kila Muislamu ana wajibu wa kuzitekeleza nguzo zote
2 Alama ya ukweli wa kiimani
Mali kimaumbile ni kipenzi na si rahisi mtu kukitoa anachokipenda isipokuwa apate kama kile au zaidi yake. Mwenye kutoa Zakaah hutaraji malipo zaidi na fadhila kutoka kwake Subhaana na huwa ni kitu kipenzi zaidi kwake.
3 Ni sababu ya kuingizwa peponi
Kwa mujibu wa aya na hadithi nyingi zinazothibitisha hivyo.
4 Hufuta madhambi
Zakaah humfutia madhambi mwenye kuitoa huku akikusudia kupata radhi Zake Allaah (Subhaanahu Wata’ala).
ADHABU YA MWENYE KUACHA KUTOA ZAKAAH
Katika mapendekezo yaliyotolewa kwenye kidadisi kuhusu Zakaah ilitajwa kuelezwa bayana athari na madhara yake kwa mwenye uwezo wa kuitoa Zakaah na hakufanya hivyo ikiwa ni kwa makusudi au kwa kutokusudia.
Mwenye kuacha kutoa Zakaah kwa makusudi huku akijua kama ni wajibu kwake basi amekana moja katika nguzo za Kiislamu na hivyo kutoka katika dini – kurtadi. Pia ni moja katika madhambi makubwa ambayo adhabu kali imeandaliwa duniani na akhera kwa kila asiyetekeleza moja katika nguzo za Kiislamu ilhali anatambua umuhimu wake.
Khalifa Abubakr Siddiyq (Allaah Amuwie radhi), aliandaa jeshi la Waislamu kwenda kupigana na Waislamu wenzi wao kwa sababu ya kuikataa nguzo hii. Na pale ‘Umar Ibnul Khattaab, (Allaah Amuwie radhi) alipomuhoji alimwambia:
فإن الزكاة حق المال, والله لو منعوني عناقا كانوا يؤدونها إلى رسول الله صلى الله عليه وسلم لقاتلتهم على منعها
Hakika Zakaah ni haki ya mali na Wallaahi kama wakinizuilia hata kwa (kamba ya) kutiwa shemere (anayofungwa mnyama kwenye pua zake) nitapambana nao kwani walikuwa wakiitoa kwa Mtume (Salla Allaahu ‘Alayhi Wasallam).
Adhabu zilizotajwa katika Qur-aan
1 Suurat At-Tawbah:
وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ
يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـذَا مَا كَنَزْتُمْ لأَنفُسِكُمْ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ
Na wale wakusanyao dhahabu na fedha na wala hawazitoi kwa njia ya Allaah wape habari za adhabu inayoumiza (inayowangoja).
Siku (mali yao) itakapotiwa moto katika Jahannam na kwa hayo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao (na huku wanaambiwa) “haya ndiyo mali mliyojimbikizia (mliyojikusanyia) nafsi zenu basi onjeni (adhabu ya) yale mliyokuwa mkikusanya”. [Suurat At-Tawbah: 34-35]
2 Aali ‘Imraan:
وَلاَ يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللّهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُمْ بَلْ هُوَ شَرٌّ لَّهُمْ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُواْ بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلِلّهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاللّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ
3 Wala wasione wale ambao wanafanya ubakhili katika aliyowapa Allaah miongoni mwa fadhila zake kuwa ni bora kwao (kufanya ubakhili). Laa ni vibaya kwao watafungwa kongwa (minyororo inayofungwa kwenye shingo) za yale waliyoyafanyia ubakhili siku ya kiama Na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Allaah. Allaah Anazo khabari za mnayoyafanya. [Aali ‘Imraan: 180]
ADHABU ZILIZOTAJWA KATIKA SUNNAH
وعن أبي هريرة رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: (ما من صاحب ذهب ولا فضة لا يؤدي منها حقها إلا إذا كان يوم القيامة صُفِّحَت له صفائح من نار, فأُحْميَ عليها في نار جهنم, فيكوى بها جنبه وجبينه وظهره, كلما بردت أعيدت له في يوم كان مقداره خمسين ألف سنة حتى يُقْضَى بين العباد, فيرى سبيله إما إلى الجنة وإما إلى النار.) رواه مسلم
Kutoka kwa Abu Hurayrah, (Allaah Amuwie radhi), Amesema Mjumbe wa Allaah (Salla Allaahu ‘Alayhi Wasallam)
Mtu yeyote aliye na hazina na wala haitolei Zakaah basi atachomwa nayo katika moto wa Jahannam na itajaaliwa kama vinoo ambavyo atapigwa navyo kwenye migongo na vipaji mpaka Allaah Amalize kuhukumu waja wake siku ambayo ni sawa na miaka elfu khamsini. Kisha ndio ataoneshwa njia yake ikiwa kama ni ya peponi au motoni. [Muslim]
Na amesema pia:
"من آتاه الله مالاً فلم يؤد زكاته مثل له ماله يوم القيامة شجاعاً أقرع له زبيبتان يطوقه يوم القيامة، ثم يأخذ بلهزمتيه -يعني شدقيه- ثم يقول: أنا مالك أنا كنزك! ثم تلا: (وَلا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّهُ مِنْ فَضْلِهِ هُوَ خَيْراً لَهُمْ بَلْ هُوَ شَرٌّ لَهُمْ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُوا بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ) [آل عمران:180]" رواه البخاري.
Mwenye kujaaliwa mali kisha hakuitolea Zakaah yake itageuzwa (mali hiyo) nyoka mwenye sumu kali ambae kichwa chake hakina manyoya na huku ana alama za vidoto viwili vyeusi kwenye macho yake. Nyoka atamzonga kwenye shingo yake na kumng’ata kwenye mashavu huku akisema: “Mimi ni utajiri wako mimi ndiyo hazina yako” Kisha akasoma: “Wala wasione wale ambao wanafanya ubakhili katika aliyowapa Allaah miongoni mwa fadhila zake kuwa ni bora kwao (kufanya ubakhili). Laa ni vibaya kwao watafungwa kongwa (minyororo inayofungwa kwenye shingo) za yale waliyoyafanyia ubakhili siku ya kiama” [Aali ‘Imraan: 180] al-Bukhaariy
Na pia anasema Mtume (Salla Allaahu ‘Alayhi Wasallam)
"ما منع قوم الزكاة إلا ابتلاهم الله بالسنين -المجاعة والقحط-" رواه الطبراني في الأوسط ورواته ثقات
Hwatojizuia kaumu na kutoa Zakaah isipokuwa Allaah Atawapa mitihani ya ukame na njaa. At-Tabraaniy katika kitabu chake cha Al-Awsat na anasema wapokezi wake ni wenye kutegemewa.
"ولم يمنعوا زكاة أموالهم إلا منعوا القطر من السماء، ولولا البهائم لم يمطروا" رواه ابن ماجه و البزار
Na hawakujizuia kaumu na kutoa Zakaah ya mali zao isipokuwa Allaah Atawazuilia mvua kutoka mbinguni na lau kama si wanyama basi (mvua) isingelinyesha. Ibnu Maajah na Al-Bazzaar
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment