Sunday, 25 December 2011

Watu Aina Saba Watakaokuwa Katika Kivuli Cha Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) Siku Ya Qiyaamah

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kuna watu saba (7) ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) atawafunika katika kivuli chake katika siku ambayo kutakuwa hakuna kivuli isipokuwa kivuli chake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)”: 1. Kiongozi Muadilifu; 2. Kijana aliyekulia katika kumcha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala); 3. Muislamu ambaye moyo wake umesehelea katika msikiti; 4. Watu wawili wapendanao kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), Kukutana kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kuachana kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala); 5. Mwanaume aliyeitwa na mwanamke mrembo kwa kutaka kufanya matendo ya haramu na akasema, “La hakika mimi namuogopa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala)”. 6. Mtu anayetoa sadaka kwa mkono wa kulia na wa kushoto usijue kitu kilichotendeka (atoae sadaka kwa siri bila ya wengine kujua kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), na 7. Mtu anayemkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa faragha na huku macho yake yakatokwa na machozi.” (Al-Bukhaariy na Muslim) Katika Hadiyth hii nzuri Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kazungumzia kuhusu vitu vidogo vya ‘Ibaadah ambavyo ujira wake ni mkubwa mno: kivuli katika siku ambayo kutakuwa hakuna kivuli isipokuwa cha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Hii inaweza kuonekana kuwa si jambo kubwa katika mara ya kwanza utakaposoma, lakini ukidhamiria katika Hadiyth ifuatayo; “Katika siku ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) atawafufua viumbe vyake vyote, jua litashushwa karibu sana na watu ambapo kutaachwa tofauti ya maili moja baina ya jua na watu ardhini. Watu watatopea katika jasho kulingana na amali zao, wengine mpaka kwenye vifundo vya vya miguu, wengine mpaka kwenye magoti yao, wengine mpaka kwenye viuno vyao na wengine watakuwa na hatamu ya jasho na, wakati yalivokuwa yanasemwa haya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliweka mkono mbele ya mdomo wake.” Imesimuliwa na Al-Miqdaad bin Aswad na imekusanywa katika Swahiyh Muslim - Juzuu ya nne (4), ukurasa wa 1487-8, nambari 6852. Na katika Hadiyth nyengine, watu wengine watatopea katika jasho “Sawa na urefu wa mikono sabini (70) katika dunia” (Al-Bukhaariy na Muslim) Nani atataka zaidi ya kuwa katika kivuli na hifadhi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika siku hii. Wacha tu tuchunguze sasa sifa na fadhila za haya makundi saba (7) ya watu ambao wanastahiki na kuadhimikiwa na nafasi hii katika siku ambayo binaadamu wote watakusanyika. “Kiongozi Muadilifu…” Sheria/Haki katika Uislamu ni muhimu sana na ni kitu ambacho kila Muislamu Kiongozi na waongozwa lazima wafuate katika kila kitu bila ya hitilafu yoyote. Sheria ni kumpa kila mtu haki anayestahiki. Waislamu au wasio waislamu, ndugu au mgeni, rafiki au adui. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema: “Enyi mlio amini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mkitoa ushahidi kwa haki. Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na ucha Mungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu Anazo khabari za mnayoyatenda.” [Al-Maaidah: 8] Hata kama tunakubali katika kanuni, tunasahau haraka kwenye kufuata. Ndio maana unaona tukizungumza kuhusu marafiki zetu na watu walio karibu nasi, tunawasifia kupita kiasi, na tukizungumza kuhusu watu kinyume na hao, hatusemi hata jema moja lao na tunayakumbuka au kuyataja mabaya yao tu. Hii imetolewa na kutupwa kabisa katika sheria/haki ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anaipenda na hutoa ujira au thawabu kubwa mno kwaye, kama ilivotajwa katika Hadiyth ifuatayo: “Yule mtenda sheria atakuwa katika kiti cha enzi kwenye mkono wa kulia wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) – na hakika mikono yote ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ipo kulia (haki) kwa wale ambao waadilifu wa sheria katika utawala wao, baina ya familia zao na kila kitu ambacho wamepewa mamlaka [Muslim]. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuagiza Abdullaah bin Mas’uud sehemu iliowazi katika mji wa Madiynah baina ya makazi na bustani ya mitende ya Answaar na aliposema Banu ‘Abd bin Zuhrah, “Watoe hapa kwetu watoto wa Umm ‘Abd (Ibn Mas’uud), akajibu, “Kwanini Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) amenileta mimi. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) hapendi wala hawarehemu watu baina yenu ambao hawatoi haki kwa watu walio dhaifu.” [At-Tirmidhiy] Kutekeleza Sheria kwa haki na uadilifu ni muhimu sana kwa mtawala yoyote, madhali yeye ndio mshika hatamu wa watu wake na yeye ndio mtoa haki wa mwisho katika sehemu husika, Kwa sababu hii, mtawala amepewa nafasi muhimu sana kama mmoja katika watu saba ambao watatunikiwa kivuli cha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) siku ya Qiyaamah. “Kijana aliyekulia katika kumcha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)…” Mwanachuoni mkubwa Ayyuub as-Sakhtiyaaniy (aliyefariki mwaka 131H) amesema, “Kutokana na mafanikio anayokuwa nayo kijana, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anamuongoza kuwa mwanachuoni wa Sunnah.” Hasan – Imesimuliwa katika Sharh Usuul as-Sunnah ya Imaam al-Laalikaa’iy (Namba 30). Kweli, ni baraka iliyoje kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa kijana ambaye ameongozwa kwenye ibada na akawa na urafiki au uongozo mzuri kwenye mambo mema, kwani kama tunavojua kuwa ni katika ujana wa mtu ambapo hukabiliwa na vishawishi vya dunia na huwa rahisi kuteleza kwenye njia ya Uislamu. Hii inakuwa dhihirifu pale tunapoana kwenye jamii zetu na tunaona hadaa nyingi za kidunia, kama muziki, michezo, vilabu mbali mbali visivo vya kheri, mambo ya fasheni na kadhalika. Hivi vyote huwa vimelenga au mlengwa mkuu katika mambo hayo tuliyoyataja hapo juu ni vijana. “Ujana huwa mara moja tu!” huwa wanaambiwa, na ndio maana Waislamu wengi siku hizi wanapoteza ujana wao kufikiri kuwa wataswali, watavaa Hijaab na kwenda kuhiji na kadhalika pale watakapofikia umri wa uzee, kama vile wana uhakikisho wa maisha marefu kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)! Ewe ndugu yangu Muislamu ni kiasi gani tunajali wasia wa mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema: “Chukua faida ya mambo matano (5) kabla ya matano (5): ujana wako kabla ya uzee wako, afya yako kabla ya maradhi yako, mali yako kabla ya ufukara wako, faragha yako kabla ya wakati utakaoshughulishwa na mambo mbali mbali, na maisha yako kabla ya kifo chako.” [Al-Haakim] “Muislamu ambae moyo wake umesehelea (umeambatana) katika msikiti…” Kuna msisitizo mkubwa katika Sunnah kwa Muislamu mwanaume kuswali msikitini na malipo yake ni ni makubwa mno. Sio tu inamwezesha mtu astahiki kivuli cha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) siku ya Qiyaamah, bali pia “…kila hatua anayochukua kuelekea msikitini hunyanyuliwa daraja moja na hufutiwa dhambi moja. Wakati akiswali, Malaika hawaachi kumuombea madhali yuko katika sehemu ya ibada na husema, Ewe Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma mrehemu mja wako huyu, Ewe Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma mhurumie mja wako huyu…” [Al-Bukhaariy] Hadiyth zote zinazowahamasisha wanaume kusehelea misikitini hazimaanishi wala hazikusudii kumuongoza mmoja kufikia timamu ya kwamba Uislamu ni Dini ambayo inatakiwa itekelezwe misikitini tu, kama watu wengi wanavofikiria. Misikiti inatakiwa iwe katika moyo wa jamii ya Kiislamu, na jukumu la wale wahusika wa msikiti ni kubwa na zito. Wao ndio wahusika wakuu wa kukaribisha stara kwa Waislamu, kuliko kuwa uwanja wa siasa na kitega uchumi kama ilivokuwa misikiti mingi siku hizi. Na tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atuepushe na mambo kama haya kutokea! “Watu wawili wapendanao kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), wakakutana kwa ajili ya Mola wao na wakatengana kwa ajili ya Mola wao…” Kuwa na upendo wa dhati kwa jili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ni moja ya milango mitukufu kuelekea kwenye mazuri ya huko akhera na ni chanzo cha kuonja uzuri wa Imani katika dunia hii. Kupendana kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) inamaanisha Muislamu anatakiwa ampende Muislamu mwenzake kwa ajili ya usahihi au uongofu wa Dini yake. Bila ya kujali rangi, mtazamo wa kisura, anavaa nini, kama ni tajiri au maskini, anatoka wapi, au pengine ukachukia kila kitu chake ila ukampenda kwa ajili ya Imani yake: Huku ndiko kupendana kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). “Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema katika Hadiyth Al-Qudsiy: “Wale ambao wana upendo wa dhati kwa ajili ya Utukufu Wangu watakuwa na nguzo ya mwangaza, watahusudiwa na Mitume na mashahidi.” [At-Tirmidhiy na Musnad Ahman] SubhanAllaah! Fikiria kuhusudiwa na Mitume aliowachagua Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) mwenyewe, na wale waliofariki kwa ajili ya njia na radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)!. Hayo ni malipo makubwa sana kwa wale wanaopendana kwa ajili ya Mola wao Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). “Mwanaume anayeitwa na mwanamke mrembo kwa kutaka kufanya matendo ya haramu na akasema “La hakika mimi namuogopa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala)…” Dunia hii imejaa vishawishi ambavyo vinaelekeza kwenye moto wa jahannam na miongoni mwa hivyo vishawishi ni vile vinavotokana na wanawake. Wanaume wengi wameelekeza mioyo na nafsi zao kwenye maangamizi ya vishawishi vya wanawake na pia ndio maana Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuonya Ummah wake mahsusi kuhusu suala hili. Akasema, “Dunia ni nzuri na ya kijani na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atakuwekeni na Atakufanyeni nyinyi kuwa mlioendelea ili Aone mutakayoyatenda. Basi Jiepusheni na ushawishi unaotokana na wanawake: Hakika mtihani wa mwanzo wa wana wa Israaiyl ulisababishwa na wanawake.” [Muslim] Ni muhimu sana kujiandaa na kujikinga kutokana na fitnah hii inayosababishwa na wanawake na vishawishi vengine vyote katika maisha kwa kumhofu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Jambo hili hakika pia limezungumziwa katika Aayah ya Qur-aan ifuatayo: “Na ama yule anayeogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake Mlezi, na akajizuilia nafsi yake na matamanio, Basi huyo, Pepo itakuwa ndiyo makaazi yake!.” [An- Naazi`aat: 40-41]. “Mtu anayetoa sadaka kwa mkono wa kulia na wa kushoto usijue kitu kilichotendeka (atoae sadaka kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa siri bila ya wengine kujua …” Hii inaeleza aina ya mtu anayeelekea katika umbali wa hali ya juu kabisa katika kujilinda na kujiepusha na Riyaa (kufanya amali njema ili watu wamuone na kumsifu). Dhambi hii kubwa inaangamiza faida ambazo zimo kwenye amali njema na husababisha adhabu kali kwa yule anayefanya jambo hilo. Ni hatari kwa kuwa ni tabia ya binaadamu kupenda na kufurahia watu wakimhimidi (wakimtukuza). Hivvo ni lazima tuwe makini sana na kuhakikisha kuwa nia zetu zinaanza na kuendelea kubakia kuwa safi kila mara tufanyapo amali njema kama kutoa sadaka. Sio kama tunavoona leo ambapo katika Misikiti yetu utakuta watu katika kipaza sauti na mabao ya matangazo yanayosema, ‘Fulani katoa kadhaa kumpa fulanikwa sababu kadhaa wa kadhaa! Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anaonya kwa kusema: “Enyi mlioamini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na maudhi, kama anayetoa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala hamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu yake pana udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa, ikaliacha tupu. Basi hawatakuwa na uweza wowote kwa walivyo chuma. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri…” [al-Baqarah: 264]. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) atukinge katika jambo hili na atuongoze katika njia za kheri! “Mtu anayemkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa faragha na huku macho yake yakatokwa na machozi.” Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametueleza: “Ingelikuwa unayajua ninayoyajua mimi, ungeli cheka kidogo na ukalia sana.” [Al-Bukhaariy] Kulia machozi sio alama ya udhaifu. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alikuwa ndio binaadamu bora kabisa kuliko viumbe vyote, alikuwa akilia na pia Maswahaba zake wakifanya hivyo hivyo. Machozi ni njia thabiti ya kuonesha uoga wetu juu ya adhabu kali za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), upendo wetu wa dhati na kweli juu yake na hayaa (fazaa) juu yake. Lakini je, ni mara ngapi tunamkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa faragha au upweke na huku machozi yakatutoka? Kiasi gani tunacheka na kufurahi kwa wingi na kulia kidogo sana? Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna kitu ambacho kinampendezesha na kupendwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kama matone mawili na alama mbili: Tone la chozi lilotoka kwa ajili ya kumwogopa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), na tone la damu lilitoka kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Na hizo alama mbili ni, alama iliyosababishwa kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), na alama iliyosababishwa kwa kutimiza moja kati ya mambo ya fardhi yaliyoamrishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)…” [At-Tirmidhiy na katika Mishkaat] Alhamdulillaah, kwa mafunzo tunayoyapata kutokana na hawa watu wa aina saba (7) waliotajwa katika Hadiyth, tumepewa alama wazi wazi za kutuongoza katika kupata starehe na ridhaa au utoshelezi. Kwa hiyo, Ndugu zangu Waislamu tujitolee na tufanye jitihada kubwa ili tuwe miongoni mwa hawa watu saba, kwa hakika watu wenye bahati watakuwa wale watakaopewa kivuli cha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika siku ambayo kutakuwa hakuna kivuli chochote isipokuwa cha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) pekee. Aamiyn

No comments:

Post a Comment