Sunday, 25 December 2011
Mke Bora:
Mtungaji: 'Aliy 'Umar 'Uthmaan
1. Tupunguze mahari, mabanati waolewe
Ili tuepuke shari, wenetu wasitiriwe
Tuwatoe kwa fahari, tuombe wabarikiwe
2. Mke alivyoamriwa, dini yetu tuisome
Kwake mefaradhiwa, sheria aziandame
Lau mja husujudiwa, mke angeabudu mume
3. Akae nyumbani kwake, amlekee Mola pekewe
Atimize wajibu wake, ibada kwa wakatiwe
Jihadi ya mwanamke, ni kumtwii mumewe
4. Binti jikalie kwako, upate kusifika
Mume ni rafiki yako, kumliwaza yataka
Mume ni moshi wa koko, usipowaka hufuka
5. Husitiri siri yake, hampi labuda maiti
Katu usiteteleke, usiwe yako hufiti
Mtu hafui demu lake, katikati ya umati
6. Siku zote vumilia, mambo ngakusonga
Nyumbayo shikilia, maisha vyema panga
Mwana elewa dunia, ni pepo ya wajinga
7. Ufanye uvumilivu, uandame ule wakati
Jikoni japo kukavu, ulimi wako dhibiti
Asokujua alie wivu, aone una mno bahati
8. Waepuke wavundifu, tunga wako muamala
Hali japo ni dhaifu, sitamauke kwa Mola
Mtu haandami lufufu, ni matumizi na kula
9. Mja hujua atokako, dhiki nana usione
Katu hujui wendako muatie Mola sinene
Siri za nyumba yako, zisikeuke kuta nne
10. Hutopata utakacho, pepo tanga uandame
Siwe nanga ubwiacho, ni hilo hilo siseme
Shukuru upawacho, simkalifishe mume
11. Mwana soma upishi, hebu wata kukoroga
Upike mule freshi, vyakula na maboga
Basi hapo mutaishi, ya kweli sio soga
12. Uwe bora muandazi, uwalishe vya tiba
Wape wanayo malezi, shirikiana na baba
Waonyeshe mapenzi, japo riziki ni haba
13. Kupunguza gharama, na uipinge isirafu
Huwa nusu ya kutuma, kujiwekea halafu
Kuyafuja mali koma, kuna maji kuwa mafu
14. Pale mukiruzukiwa, ukumbuke na ukame
Na dini tumeusiwa, muonee utungu mume
Usipike visoliwa, mwana israfu ukome
15. Tunga mali ya mumeo, ni akibayo usivuju-usifujeni
Siri ziweke pekeyo, sinene hata iweje
Saza simalize leo, kesho shida zisije
16. Jilinde na machafu, umakinike uolewe
Uepuke na uvundifu, wendapo usitahiwe
Sifa ya mke ni upofu, asoona illa mumewe
17. Mke mwema ni kiziwi, haoni wala hasikii
Asowasikiza wawi, raha mume kumtwii
Na waovu hahadawi, uchafu hafikirii
18. Mke mwema ni kiduko, uzito kutiwa chuki
Huviepuka vituko, hamtii mume dhiki
Katu hana papatiko, mumewe hambanduki
19. Mke mwema huwa bubwi, asonena illa kheri
Si umbile la lumbwi, kisema hutafakari
Kinyume na chubwi, aolea juu ya bahari
20. Mke sawa awe kiwete, hakeuki kizingiti
Katu hendi kokote, akikatzwa huketi
Wa nidhamu saa zote, haupotezi wakati
21. Mwana siwe kirango, buibui kuwa ruhusa
Katu sinene urongo, hilo ni kubwa kosa
Lituze lako bongo, waume wawapi sasa?
22. Mwana guu silivute, bila ruhusa ya mume
Kikatazwa usitete, shatani usiandame
Radhi ya Mngu upate, katu nawe silalame
23. Utunge sana ulimi, siyanene yakaraha
Hututongea ndimi, tukazikosa na raha
Kama kweli umneni, basi nena ya furaha
24. Na mumeo mukiteta, sio mbele ya watoto
Suluhu nawe tafuta, wala usione uzito
Msamaha kishapata, ndio ulifumbe jito
25. Usimuinulie sauti, kimzungumzia mume
Ikitokea tafauti, siropokwe jipime
Alozalikana binti, ni mtele uso ndume
26. Saa zote jieke safi, japo ni kopo la maji
Husifika mwanamke, upambe kiwa kipaji
Mume hata atosheke, awe nde si mwendaji
27. Pale jito lifikapo, pawe swafi mwilini
Kila nyote mukaapo, utumie lugha laini
Hata kenda endapo, roho iwe nyumbani
28. Nguo japo tambara, uchachage lazima
Bora upate sitara, dhikizo kutosema
Usimame sana imara, usitikisike daima
29. Simnukishe uvundo, aingiapo nyumbani
Ayaone kwa vitendo, ustaarabu wa pwani
Umuoneshe na pendo, akiwa nde na ndani
30. Ujifukize na nyudi, jikwatue ndio ada
Ujiweke maradadi, kwa viluwa na poda
Mumeo roho iburudi, nakuusia ewe dada
31. Mama imekulazimu, una wajibu duniani
Ulichozaa muhimu, yatie sana akilini
Mama ndiwe mwalimu, wa wanayo nyumbani
32. Walee wanayo vyema, kwa misingi ya dini
Waonee sana huruma, siwatese masikini
Uhusiano uwe mwema, watakufaa mbeleni
33. Mpendee mume nduze, ulitunge na jinale
Mume usimpeleleze, yuwatoa ngapi kule
Muhimu atakeleze, katu haramu musile
34. Mtie mume urafiki, hata nde kusimueke
Ili waja wanafiki, mabega yawashuke
Ni wajibu yako haki, mtu kuzatiti chake
35. Marafikizo kwanda, watuje kwa makini
Watague kama tunda, pale wendapo sokoni
Uepuke asokupenda, kumjaza nyumbani
36. Watunge sana watu, usije matozi kulia
Kuna wasojali kitu, na wenye mbaya nia
Kitanda asisubutu, mwengineo kulalia
37. Linda faragha yako, wasione watu wote
Uwe na mema mashiko, uyafuate kwa kite
Mke chumbani kwako, mamnuu kwa yoyote
38. kama una uzuri- kama una uzuri bora, hutomshinda Hawa
Wapili mrembo Sara, Ibrahimu alomkewa
Vipusa walo na sura, na radhi za Moliwa
39. Mwana usiteteleke, usiwe nawe kama hao
Jikaze mno umueke, mume ubora alonao
Wele wao wanawake, wasotwii waume zao
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment