Sunday, 22 January 2012

Hatari Ya Kuihama Qur-aan:

Anasema Allaah سبحانه وتعالى :
((وَقَالَ الرَّسُولُ يَا رَبِّ إِنَّ قَوْمِي اتَّخَذُوا هَذَا الْقُرْآنَ مَهْجُورًا))

((Na Mtume amesema: Ee Mola wangu! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur-aan ni kitu kilichohamwa (kilichoachiliwa mbali)))
[Al-Furqaan: 30]

Allaah سبحانه وتعالى Anatuambia jinsi Mtume صلى الله عليه وآله وسلم Alivyokuwa akilalamika kuwa watu wake wameihama na kuipuuza hii Qur-aan. Makafiri Quraysh walikuwa hawataki kusikiliza Qur-aan, na ilipokuwa ikisomwa walikuwa wakizungumza upuuzi au kuzungumza kwa sauti za juu mazungumzo mengine ili wasiisikie kama Anavyosema Allaah
سبحانه وتعالى :

((وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لاَ تَسْمَعُوا لِهَذَا الْقُرْآنِ وَالْغَوْا فِيهِ لَعَلَّكُمْ تَغْلِبُون))

((Na waliokufuru walisema: Msiisikilize Qur-aan hii, na timueni zogo, huenda mkashinda)) [Fusswilat: 26]

Hali hii ya kuipuuza Qur-aan vile vile iko miongoni mwa Waislamu hali kadhalika, ingawa Waislamu tofauti yake ni kuwa wameiamini na sio kama Makafiri Quraysh ambao ilikuwa ni dhaahiri kuwa waliikanusha na kutoiamini.

Wafasiri Wa Qur-aan wameifafanua Aayah hiyo ya kwanza inayosema,

((إِنَّ قَوْمِي اتَّخَذُوا هَذَا الْقُرْآنَ مَهْجُورًا))

((Hakika watu wangu wameifanya hii Qur-aan ni kitu kilichohamwa (kilichoachiliwa mbali)))

kwamba: kuihama na kupuuza Qur-aan inawahusu watu wa aina zifuatazo:
1. Wasioisoma kabisa.
2. Wanaoisoma lakini hawajifunzi maana yake.
3. Wanaoisoma na kujifunza maana yake lakini hawafuati maamrisho yake na hawajiepushi na makatazo yake.

Kuihama Qur-aan na kuipuuza ni hatari kubwa kabisa na Mola wetu Mtukufu Ametuonya na Kututisha kupitia Aayah nyingi za Qur-aan.
Miongoni mwa maonyo hayo ni kwamba mja atakuwa na maisha ya dhiki na hufufuliwa siku ya Qiyaamah akiwa kipofu kama ifuatavyo:

((وَمَنْ أَعْرَضَ عَن ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكًا وَنَحْشُرُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَعْمَى)) ((قَالَ رَبِّ لِمَ حَشَرْتَنِي أَعْمَى وَقَدْ كُنتُ بَصِيرًا)) ((قَالَ كَذَلِكَ أَتَتْكَ آيَاتُنَا فَنَسِيتَهَا وَكَذَلِكَ الْيَوْمَ تُنسَى))

((Na atakayejiepusha na mawaidha Yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Qiyaamah Tutamfufua hali ya kuwa kipofu)) ((Aseme: Ee Mola wangu, mbona Umenifufua kipofu, nami nilikuwa nikiona?)) (Allaah سبحانه وتعالى) Atasema: Ndivyo vivyo hivyo. Zilikufikia ishara Zetu, nawe ukazisahau, na kadhaalika leo unasahauliwa)) [Twaaha: 124-126]

Ndugu Waislamu tunaona hatari ya kuipuuza Qur-aan na kuihama basi na tujitahidi kuisoma, kujifunza maana yake na kufuata maamrisho yake na kujiepusha na makatazo yake ili tuwe miongoni mwa wale Aliowasifu Allaah سبحانه وتعالى katika hii Qur-aan kuwa wanaisoma 'ipasavyo kusomwa' katika kauli Yake:

((الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَتْلُونَهُ حَقَّ تِلاَوَتِهِ أُوْلَئِكَ يُؤْمِنُونَ بِهِ))

((Wale Tuliowapa Kitabu, wakakisoma kama ipasavyo kusomwa, hao ndio kweli wanakiamini)) [Al-Baqarah:121]

Zifuatazo ni kauli za Maswahaba رضي الله عنهم kuhusu 'kuisoma ipasavyo’

Ibn Mas'uud رضي الله عنه: "Naapa kwa Yule Nafsi yangu iko mikononi Mwake, Tilaawa ya kweli ni kufuata yaliohalalishwa na kuacha yaliokatazwa, kusoma kama ilivyoteremshwa, kutokubadilisha maneno katika sehemu zake na kutokuifasiri vingine na ilivyopasa kutafsiriwa" [At-Twabariy 2.567]

Ibn 'Abbaasرضي الله عنهما : "Wenye kuhalalisha yaliyo halali na kukataza yalioharimishwa na hawabadilishi maneno yake".[At-Twabariy 2.567]

'Umar bin Al-Khattwaab رضي الله عنه: "Ni wale ambao inaposomwa Aayah na inapotajwa Rehma wanamuomba Allaah سبحانه وتعالى Rehma Yake, na wanaposoma Aayah inayotaja adhabu, wanajikinga kwa Allaah سبحانه وتعالى nayo". [Al-Qurtubiy 2:95]

Kauli ya 'Umar bin Al-Khattwaab رضي الله عنه: ni kama ilivyokuwa desturi ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipokuwa akipita katika Aayah ya Rehma alikuwa akimuomba Allaah سبحانه وتعالى Rehma Yake,
na alipokuwa akisoma Aayah ya adhabu alikuwa akijikinga kwa Allaah سبحانه وتعالى na adhabu.
Maneno yafuatayo ni ya busara ya Mshairi aliyesema kuhusu Qur-aan. Nasi tunamuomba Allaah سبحانه وتعالى Atujaalie kuandamana na Kitabu Chake hiki ambacho ndio uongofu wetu kamili na mwangaza utakaotutoa katika kiza na kutuingiza katika Nuru (mwanga), na ndio itakayokuwa sababu ya kufuzu kwetu Duniani na Akhera.

Aamiyn.

3 comments:

  1. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  2. kazi mzuri kaka Mungu akubariki kwa juhudi zako

    ReplyDelete
    Replies
    1. ASANTE SANA SAA UBUGUVU, MUNGU ATUJAALIYE TUWE WENYE KUKITUMIKIA KITABU CHAKE KITUKUFU.

      Delete