MWONGOZO WA KUJISOMEA:
Kujifunza kwa ufanisi ni jambo muhimu sana. Sisi Tukiwa kama wanafunzi, tunasumbuliwa na matatizo mengi ya kiuanafunzi, ambayo sote tunayajua. Hata hivyo, pongezi kwa Uongozi wa TSU EGYPT kwa kuamua mwaka huu uwe mwaka wa kuandaa na kuwasilisha tafiti za kielimu zinazohusiana na maswala mbalimbali yanayowagusa watanzania. Nyaraka hizi zina shabaha ya kuchangia katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo la Kujifunza kwa ufanisi.
Kwa hakika, wengi wetu, tunachukulia kuwa, Kujifunza ni kwenda vyuoni au madarasani. Hayo ni mojawapo ya mawazo finyu kuhusiana na kujifunza, kwani kujifunza kuna maana pana zaidi kuliko ile ya kwenda madarasani.
Ili tusirefushe sana! Kujifunza kunakusanya kwenda madarasani na kuwasikiliza wahadhiri kwa makini, kujisomea vitabu na makala mbalimbali kwa ufanisi, kusikiliza marafiki, walimu, wazazi, wataalamu, kutazama video, sinema, kufanya utafiti (bahthi/research), kufanya kazi za nyumbani, kufanya mazoezi, kufikiria njia za kutatua matatizo, kufikiria njia za kujiletea maendeleo, nk.
Kwa faida ya msomaji/msikiliza: Jaribu kuweka akilini huu ufahamu mpana wa kujifunza kwani hilo litakusaidia kujifunza kwa ufanisi na kwa maendeleo endelevu.
Baada ya utangulizi huu linaibuka swali! Mbinu za kujisomea ni nini?
Mbinu za kujisomea ni mfumo au njia za kumfanya mtu ajifunze kiwepesi na kwa ufanisi zaidi. Tunapenda ifahamike kuwa hizi Mbinu za kujifunza sio kitu mbadala cha kuacha kutoa bidii katika kujifunza.
Kwa hakika juhudi katika kujifunza ni jambo la muhimu sana. Ama umuhimu wa mbinu za kujifunza ni kuwepesha na kurahisisha suala la kujifunza. Pia zinaokoa muda na nguvu za mwenye kuzitumia.
Imesemekana kuwa: Watu wanajifunza na kufahamu vizuri pale wanapotekeleza kivitendo yale wanayojifunza.
Kwa mfano ukimfundisha mtu kuendesha baiskeli atajua haraka kama atakuwa amepanda baiskeli sio maneno matupu! Au kama vile kumfundisha mtu kuogelea akiwa nchi kavu kwa kweli hatoweza kujua kuogolea. Pia ieleweke kuwa kila mtu anajifunza kwa njia yake anayoipenda na kuona inamfaa.
No comments:
Post a Comment