MAFUNDISHO YA SHULE KWA MPANGILIO WA KIISLAMU:
“Uislamu ni tajiri sana kwenye upande wa elimu na hakuna elimu ambayo imeiacha. Hivi karibuni tutatoa mwelekeo wa uislamu kwenye elimu, na tutanukuu maneno ya Imaam Ghazali kwenye Ihyaa Uloomud-Diin. Tutatunukuu hapa sehemu ndogo kwa kifupi sana, Imaam Ghazali anasema elimu imegawika kuwa lazima kwa kila mmoja, na elimu iliyokuwa lazima kwa kikundi cha watu, elimu iliyokuwa makruuh na elimu iliyokuwa mubaah na elimu iliyokuwa haramu.
Katika elimu iliyokuwa lazima, kasema si lazima mtu ajue milango yote ya sheria bali ajue kila kinachotakiwa katika muda na hali alionao, akasema kwa mfano si lazima kujua hukumu za Hijja kama hana uwezo na wakati wa Hijja haujafika.
Kisha akaendelea kueleza na akasema watu wanahangaika kusoma maelezo ya undani wa sheria na mifano ya mas-ala ambayo hayatokei ila kwa nadra na wakati mjini kwao hakuna daktari wa kike Muislamu wa kutibu wanawake wa kiislamu, na ni jambo la lazima kwa wakazi wa mji na kama halijafanyika wanapata madhambi wakazi wote.
Kwa hiyo ni wazi kuwa baadhi ya elimu tunazoziita za dunia ni lazima tujifunze kwa amri ya dini yetu, na tusipofanya hivyo tutaingia kwenye madhambi makubwa. Maelezo zaidi tutayatoa kwenye makala zetu zijazo.
Wajerumani walivyokuja Tanganyika, wakaona wasomi zaidi ni Waislamu, wanajua kusoma na kuandika, wanajua hesabu na wanatumia tarakimu za kiarabu kwenye maandiko yao, hata lugha ya Kiswahili ilikuwa wanatumia maandishi ya kiarabu. Wakawaajiri hawa kwenye mahakama, na nafasi za Serikali.
Mwingereza alikuja na makusudio yake, ya kuuvunja uislamu na kuwadhoofisha Waislamu, akajenga mashule na kuweka masharti anayetaka kujiunga lazima awe mkristo, ili ajiunge, ndiyo wakati tuliopata majina ya Augostino Saidi na mengineyo.
Waliopenda dini yao, wakachukia masomo ya kizungu na kukataa kupeleka watoto wao mashuleni, ili wasiwe wakristo, wakahifadhi dini yao, lakini ikajijenga tabia ya kuchukia elimu za kizungu.
Kwa hakika elimu hizi si za kizungu, ni za Waislamu wenyewe na zinarudi kwao wenyewe, Waislamu waliendeleza elimu na teknolojia, na wafalme wa kiislamu waliwapa zawadi kubwa kubwa wasomi waliovumbua mashine mpya, na zawadi ya kanisa ilikuwa ni kuwaua wanasayansi.
Hapo ndipo wakazi wa nchi za kizungu wakaamua kuweka mbali dini na sayansi & Teknolojia. Kitu hicho hakipo kwenye Uislamu. Ndiyo elimu ya secular ilipoanza.
Tukirudi kwenye Tanganyika, nafasi za Serikali zikaanza kuchukuliwa na wakristo, na wakaendelea kupata nafasi hizo, hadi Waislamu walivyoanzisha TANU, hawakuwa na Muislamu wa kushika nafasi ya juu kabisa na kumweka mkristo kwenye nafasi hiyo, na hatimaye wakristo wakaendelea kutawala.
Hiyo ni historia, tusiisahau, lakini pia isiwe ni sababu ya kutupia lawama zote kwa historia, sisi tumefanya nini kuibadili historia hiyo? Waislamu bado kwa asilimia kubwa sana wanachukia elimu za kizungu, na wana hiari wawasomeshe madrasa tu, wasipate elimu za kizungu, au wawasomeshe elimu za kizungu na wasipate elimu za dini, kama wanavyotoka Waislamu wengi hata kwenye shule tunazoziita za Kiislamu.
Hakuna sehemu ambapo tumeziweka hizi elimu za kizungu ambazo kwa hakika si za kizungu ziendane na mafunzo ya Uislamu, na kama zipo shule hizo labda hatuzijui.
Kwa kweli njia hizi mbili tumeziweka mbali sana, na hatujajenga njia ya kuzikutanisha, Wanasayansi wakubwa wa kiislamu, wanaanza vitabu vyao kwa Bismillahi, kumshukuru Mwenyezi Mungu na kumswalia Mtume - Rehema na Amani zimshukie - na bado wanabaki kuwa wanasayansi na wavumbuzi na wazungu wanaiba uvumbuzi wao na kusema wamevumbua wao, bali kushika kwao dini kunawafanya wawe wanasayansi wakubwa zaidi.
No comments:
Post a Comment