Tuesday, 31 January 2012

NAMNA YA KUPANGILIA WAKATI:

Kupangilia wakati ndio njia ya mafanikio. Vitabu vya dini vinahimiza watu wawe na ratiba ya mambo ya ibada na mengineyo. Mtu asiye na ratiba hana mafanikio maishani vyovyote atakavyokuwa.
Kwani kujipangia ratiba ni sawa na methali ya Kiswahili isemayo “Mali bila ya daftari hulika bila habari” wakati ni mali, na mtu asiye na ratiba mara nyingi hupoteza wakati mwingi bila habari! Ukijiwekea ratiba nzuri itakusaidia kutekeleza mambo yako kwa ufanisi. Lengo la kurasa hizi ni kutoa mwongozo juu ya namna ya kujipangia ratiba ya kila siku.

NAMNA YA KUPANGA RATIBA.
1) Kwanza kabisa, fahamu kile unachokihitaji kukitenda kwa siku nzima. Kisha jipe muda maalum wa kukamilisha kila tendo.
2) Jaribu kuweka uwiano mzuri (balanzi) yaani jipe muda wa kutosha kwa ajili ya kazi, mapunziko, kutazama TV, kuongea na marafiki, kupiga soga katika utandawazi, kufanya mazoezi, muda wa ibada, kutembelea ndugu, nk.
3) Kwa muda wa kujifunza, jaribu kuupangia ratiba katika nyakati ambazo unakuwa mchangamfu na hakuna vishawishi kama mechi za soka, michezo ya kuigiza, na kitu chochote upendacho kukifanya kwa wakati huo.
4) Jitahidi utenge muda wa kujifunza takriban kila siku, chagua muda kwa kila siku wa kujifunza sio mbaya kama kutakuwa na mapunziko siku moja au mbili kwa wiki.
5) Kila siku jipe muda huru usio wa kufanya kitu chochote, ndani ya muda huo waweza kufanya lolote bila kudhuru maslahi yako.
6) Jilazimishe kufuata ratiba yako.

NAMNA YA KUJIANDAA NA MTIHANI.
Maandalizi bora kabla ya mtihani ni kujisomea kwa njia zinazoleta matunda mazuri. Na zifuatazo ni baadhi ya njia zinazoweza kuleta mafanikio katika mitihani:
1. Jiandae mapema kwa ajili mtihani.
2. Jisomea kila siku kwa mujibu wa ratiba.
3. Ikiwezeakana jisomee na wenzako (weka kambi ya mtihani).
4. Pitia vizuri masomo yote.
5. Hakikisha unapata muda wa kutosha wa kupunzika ili usipate kihoro au homa ya mtihani.
6. Kula vizuri, fanya mazoezi ya mwali ili uwe mchangamfu.
7. Usiku wa mtihani jisomee kwa muda wa masaa yasiozidi matatu, kisha pumzika vizuri na ulale kiasi cha kutosha.
8. Fika mapema katika chumba cha mtihani, robo saa kabla ya kuanza mtihani.
9. Soma vizuri karatasi ya mtihani kwa ukamilifu, na jaza sehemu husika kama inavyotakikana. Usisahau, kuandika namba ya mtihani, jina, tarehe na mambo yote muhimu.
10. Hakikisha unasoma maswali kikamilifu na kuyaelewa vizuri na kama hujayaelewa muulize msimamizi akupe ufafanuzi.
11. Anza kujibu maswali mepesi kabla ya magumu, kama taratibu za mtihani zinaruhusu kufanya hivyo.
12. Baada ya kumaliza kujibu maswali yote, tafadhali yapitie majibu yako yote kwa ukamilifu.
13. Usiwe na pupa ya kutoka nje ya chumba cha mtihani.
14. Soma kwa mara ya mwisho majibu yako,na utakapokuwa na uhakika ya ulichokiandika peleka karatasi yako kwa msimamizi wa mtihani na tia saini ya kuhudhuria.

No comments:

Post a Comment