NAMNA YA KUISHUGHULIKIA MISAMIATI MIGUMU:
Kwa hakika wanafunzi wa kigeni (yaani wale wanaojifunza kwa lugha zisizo za asili yao) wanakabiliana na changamoto za maneno magumu. Ili kujaribu kutatua tatizo hili, karatasi hizi zimejaribu kuanisha baadhi ya njia za kumsaidia mwanafunzi aweze kutatua tatizo la misamiati migumu kwa upande wake. Kwanza kabisa kabla ya kuelezea namna ya kupata maana za maneno magumu tunapenda tuzingatie yafuatayo.
MAMBO YA KUZINGATIA:
1. Usipendelee kutafuta maana ya maneno magumu katika kamusi kwani kamusi linaweza kukukatiza katika kusoma kwako. Tafadhali jaribu kutumia muktadha wa maneno (mtiririko wa tungo/sentesi) kujipatia maana ya maneno magumu kwani hilo litakusaidia kuendelea na kusoma bila kukatisha.
2. Unapopata maana ya neno kwa kupitia muktadha wa maneno, tafadhali liweke alama kisha, ukimaliza kusoma, litazame hilo neno katika kamusi na ulinganishe maana uliyoipata na ile ya katika kamusi. Kama itawezekana tumia kamusi maalum za istilahi za somo husika.
3. Kama hukufanikiwa kupata maana ya neno kupitia njia ya muktadha wa maneno, hapo ndipo unapotakiwa kutumia kamusi.
Baada ya kuona mazingatio haya, sasa tutazame njia za kupata maana ya maneno magumu.
A: Njia za kupata maana ya maneno magumu:
I. Kwanza liwekee alama neno gumu kisha soma aya/ibara nzima hapo unaweza kupata maana yake. Na kama hujaipata, jaribu kuendelea na kusoma huenda maana yake ukuipata katika mistari ya mbele.
II. Kutumia kamusi. Ukiwa umeshindwa kabisa kupata maana ya neno kutokana na maelezo yaliyoandikwa katika kitabu husika, tumia kamusi kwa umakini, kwani mara nyingi kamusi inatoa fasili mbalimbali za neno husika.
B: Kupata maana ya neno kwa kupitia viashirio vya muktadha:
I. Wakati unasoma kitabu kwa lugha ya kigeni kisha ukakumbana na neno gumu, njia sahihi ya kutambua maana ya neno hilo ni kwa kupitia viashirio vya muktadha wa maneno.
II. Na muktadha wa maneno maana yake ni mazingira ya neno katika tungo au sentesi yenye kuonesha uhusiano wake na maneno mengine. Kwa Mfano neno meza kwa wale wasio waswahili, likitokea katika sentesi kama hii:
Tafadhali usikae juu ya meza. Hapa muktadha unaanisha kuwa neno meza hapa lina maana ya nomino (jina) la samani/fanicha iitwayo meza. Wala halina maana ya meza kitenzi (kitendo) cha kula na kumeza kitu kinacholiwa.
III. Viashirio vya muktadha wa maneno maana yake ni maneno mengine yaliyopamoja na hilo neno gumu katika tungo. Tukichukulia mfano uliopita utaona maneno usikae juu ya yanaashiria samani/fanicha. Wala hayaendani na neno meza kwa maana ya kumeza chakula.
AINA ZA MUKTADHA WA MANENO.
Fasili:
Wakati mwingine sentesi zinatoa fasili ya neno gumu. Mfano: ukikuta imeandikwa Kompyuta ni mashine ya umeme inayohifadhia na kuchanganua taarifa zilizoingizwa. Kwa hakika hii si fasili ya kamusi lakini inakupatia maana na matumizi ya hilo neno kwa hapo lilipo.
Mifano:
Wakati mwingine neno gumu linafafanuliwa kwa kupigiwa mfano ambao unaweza kukupatia maana ya neno husika. Mfano: Kipa wa Ruvu staa apunguze mbwewe, kama za kuchezacheza na mpira katikati ya mstari wa goli, na kujifanya hakuuona mpira, kudaka kwa mkono mmoja na kujifanya kateleza.
Ufafanuzi:
Kutoa maelezo ya neno husika. Mfano: Mwanafunzi mchecheto, yaani yule anayejikojelea kwa kuhofia mtihani anapaswa apewe ushauri nasaha.
Visawe: (mutaraadifaatu/sinonim)
Kisawe ni moja kati ya maneno mawili au zaidi yanayokaribiana sana kimaana. Mfano: Inasemekana huyo Mwizi hakutambua au hakujua kama nyumba ile inalindwa kwa kamera maalum.
Kwa ibara nyingine:
Ibara ni kifungu cha maneno au habari iliyokamilika, mfano: Tume ya haki za binadamu imefichua nyeti za mauaji ya kimbari, kwa kuziweka wazi siri za mauaji hayo.
Vinyume:
Kinyume ni neno lenye kukinzana na neno lingine. Mfano: mtu mwenye huzuni hana furaha hata kidogo.
Kutafakari:
Watu wengi wanapata kihoro wanapokutana na simba mbugani. Mtu anayetatafakari sana anaweza kujua maana ya kihoro kwa ktazama muktadha wa tungo hii.
Pia unapaswa kuzingatia muktadha wa neno wakati unapotazama fasili yake kutoka katika kamusi.
Na kama hujapata maana ya neno tafadhali litazame katika katika kamusi.
Nashukuru sana kwa yale uliyoandika. Mimi kama mwanafunzi wa mara kwa mara wa kiswahili, kuanzia miaka 27 iliyopita, daima nimeona umuhimu na thamani kubwa wa kujitumbukiza katika maandishi magumu - yaani kugonga kichwa katika kusoma. Hata ikiwa asilimia kubwa ya maana yaliyomo inanipita, naendelea tu, nikijaribu kukamua yale magumu, maana yao yaanze kutoka kwa msaada ya muktadha ya maneno na sentesi ya jirani. Na yale yanayonishinda kabisa yanendelea kunikera kichwani, mpaka siku moja, yakitumika katika muktadha ama mazingira tofauti, napata kuyakamata. Nimekuta mara nyingi, nikienda moja kwa moja kwenye kamusi na kupata maana ya neno kwa urahisi, haikai kwenye kumbukumbu.
ReplyDelete