Tuesday, 31 January 2012

NAMNA YA KUJISOMEA VITABU VYA KIADA (SHULE):

Suala la kujifunza kwa kiasi kikubwa linafungamana na kusoma vitabu, kwa hiyo, tumeonelea tuzungumzie suala la kujisomea vitabu vya kiada kwa njia ya ufanisi zaidi.
Kwa bahati mbaya wanafunzi wengi wanajisomea vitabu vya kiada kama wanavyosoma vitabu vya riwaya au visa. Yaani wanaanza kusoma ukurasa wa kwanza na kuendelea kusoma moja kwa moja hadi ukurasa wa mwisho. Wakati kwa hakika hii si njia nzuri ya kusoma vitabu vya kiada. Kwani vitabu vya kiada vimeandikwa kwa lengo la kufundisha masomo yaliyomo ndani yake. Na vitabu vya kiada vimegawanywa kwa sura.
Na kila sura imegawanywa katika vitengo, na kila kitengo kina anuani yake. Na hii ni tofauti na vitabu vya riwaya ambavyo vimeandikwa kwa mtiririko mmoja kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Kwa hiyo yapasa kuzingatia kuwa anuani za vitabu vya kiada ni nukta muhimu zinazoonesha kitabu kinafundisha nini na katika ukurasa gani. Kwa hiyo, ni jambo zuri kusoma vitabu vya kiada kwa njia maalum kama walivyoibainisha wataalamu.

Njia tuliyoichagua kwa ufipisho inaitwa (KUSUKH), na kirefu chake ni:
• K ----- Kagua:
• U ----- Uliza:
• S ----- Soma:
• U ----- Uliza:
• K ---- Kariri:
• H ---- Hakiki:

Jinsi ya kuitumia njia ya KUSUKH
1. Kagua: Kabla ya kuanza kusoma, tumia dakika mbili tatu kukagua kile utakachosoma. Hapa tunamaanisha kuwa, soma anuani zote za kifungu utakachokisoma.
Pia hakikisha unasoma muhtasari wa kifungu hicho kama upo. Vilevile soma maswali ya kujikumbusha yaliyoambatanishwa na kifungu hicho kama yapo. Faida ya kufanya hivyo ni kupata fikra ya kile utakachokisoma. Kumbuka faida za kukagua kitu kabla ya kukitumia.
2. Uliza: Baada ya kukagua, hatua inayofuata ni kuunda maswali ya kukusaidia kusoma kwa ufanisi. Na namna ya kuunda hayo maswali ni kama ifuatavyo: Geuza kila anuani iwe swali. Unaweza kuuliza kwa kutumia maneno yafuatayo: Vipi, lini, wapi, nani, inahusu nini, inafanya nini, muda gain nk. Kwa hakika ukibadilisha anuani na kuzifanya kuwa maswali, hilo linakusaidia kutambua wataka kufanya nini na kwa wakati gani.
3. Soma: Hatua ya tatu unatakiwa usome kwa makini kifungu chote ili upate majibu ya yale maswali uliojiuliza katika hatua ya pili.
4. Uliza: Baada ya kusoma, unda maswali mengine yanayohusiana na ufafanuzi uliotolewa katika kifungu. Kwa hakika maswali yanakupa changamoto za kufahamu na kukumbuka kile ulichokisoma.
5. Kariri: Katika hatua hii, unatakiwa uyarudie yale maswali uliyoyatengeneza pamoja na majibu yake uliyoyapata katika kusoma kifungu husika. Yaani soma maneno yale yale kimoyomoyo au kwa sauti au fanya vitendo vile vile mara kwa mara, rudia rudia.
Ni vizuri kuandika kwa ufupi maswali na majibu ya kifungu husika, kwani imethibitika kuwa kuandika kunasaidia kufanya mtu ashike vizuri zaidi kile alichokisoma au kukisikia. Pia waweza kutumia maandishi hayo kwa kujiandaa na mtihani yakiwa ndio ufupisho.
6. Hakiki: Hatua ya mwisho ni kufanya uhakiki wa kile ulichojifunza kwa njia ya kusoma. soma maandishi kwa kuyachambua na kufafanua mambo mbalimbali yaliyomo. Funika kitabu na karatasi ya majibu, kisha jiulize yale maswali ya kifungu cha pili, na jaribu kujipima je, unaweza kuyajibu? Kama jibu ni ndio hongera, hata hivyo soma tena katika kitabu ili kuhakikisha kweli umejibu sahihi. Kama jibu ni hapana bado una nafasi, rejea kusoma kurasa za majibu yako na kitabu ili kujiimarisha.

VIDOKEZO KATIKA KUTUMIA NJIA YA KUSUKH.
1. Tumia akili katika kuunda maswali, jiulize maswali ya msingi sio mzaha mzaha, uliza maswali, kabla na baada ya kusoma.
2. Uliza maswali ya kifungu chote.
3. Kabla hujaanza kuandika majibu ya maswali uliyojiuliza, hakikisha umeshasoma kifungu chote.
4. Andika kwa kutumia maneno yako, yaani kwa ufahamu wako. Pia fanya vifupisho kwa mtindo utakaouonelea kuwa unakufaa.
5. Usijihangaishe kwa kuandika majibu marefu, bora kuandika maneno mawili matatu yanayokukumbusha tu, kwani wewe hurudii kuandika kitabu!
6. Kumbuka kuwa hayo majibu na ufupisho ni wako, kwa hiyo usihofu kuwa watu wengine hawatoufahamu.

No comments:

Post a Comment