SOLUHISHO KWA MADRASA ZETU:
- Ni vigumu kuliondoa tatizo hili kwa kulifanya jukumu hilo kuwa la watu Fulani tu.
Mfano, kulifanya liwe jukumu la masheikh tu, au jukumu la walimu tu, au la wazazi tu. Inapaswa kuwa ni tatizo linalomgusa kihisia kila muislam.
- Kwa hakika elimu hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya uislam na waislam kiimani(kiitikadi), kitaaluma, kielimu n.k.
Mfumo.
- Kuna haja ya kuudurusi mfumo wa elimu ya madrasa na kuangalia namna ya kuuendeleza na kuuboreha kwa manufaa ya kizazi cha kiislam.
- Mfumo wa madrasa zetu uendane kabisa na haja iliyopo katika jamii kwa lengo la kuwaendeleza watoto kitaaluma.
Walimu.
- Kuwepo na mpango maalumu wa kuwaendeleza walimu kielimu, kitaaluma na kiuchumi ili kuwaongezea hari ya kujituma na kutoa jitihada zote kwa ajili ya maendeleo ya taasisi hii muhimu, “madrasati”.
Mfano:
Kuwepo kwa makongamano na semina ili kuwawezesha walimu kushirikiana katika ujuzi na mbinu za kufundishia na kuendeshea madrasa zetu.
- Walimu wawe wabunifu kiuchumi ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuendeleza madrasa zetu.
- Walimu wasijione kuwa wao ni waislam au watu wa daraja la chini sana kimaisha. Bali wajione wao ni watu muhimu kabisa katika jamii na kazi yao ni jukumu lao si jukumu la mtu Fulani na wala hawafanyi kazi hiyo ili tu kuwaridhisha watu Fulani bali ili kumridhisha allah (s.w).
Jamii ya Kiislam.
- Ifanye fikra juu ya jinsi ya kuboresha na kuendeleza madrasa zetu na watoto wetu katika taaluma muhimu za kiislam.
- Jamii nzima ieleweshwe juu ya nafasi sahihi ya Madrasa na Elimu ya Madrasa kwa maisha ya Waislam nchini.
Taasisi za Kiislam.
Zishirikiane kuona jinsi ya kutatua matatizo hayo.
TAALUMA MUHIMU KWA WALIMU WA MADRASA:
Kila nyanja inahitaji taaluma Fulani ili kuifanya nyanja hiyo iwe imara, bora, makini na yenye manufaa kwa maisha na ummah kwa ujumla. Hata Mitume (rehma na amani za Allah ziwafikie) walipewa taaluma maalumu kwa kazi zao. Katika maisha yetu tunahitaji taaluma zinazowezesha watu kutekeleza majukumu yao katika jamii na mazingira wanayoishi.
Mfano:
Mwalimu wa madrasa anahitaji taaluma juu ya;
(i) Uendeshaji wa madrasa.
(ii) Ufundishaji.
(iii) Saikolojia ya watoto na malezi.
(iv) Taaluma inazofundisha kama vile Fiqih, Tareikh, Qurani, Kiarabu, Tawhiid, Sirah, Akhlaq n.k.
Njia za kufundishia (Muhtasari)
Zipo njia kadhaa Bwana Mtume (s.a.w) amekuwa akizitumia katika kufundishia watu. Pia Quran imeeleza njia kadhaa kwa ajili ya ufundishaji. Kwa muhtasari njia hizo ni pamoja na hizi zifuatazo.
(a) Simulizi (Narration)
- Hii ni njia ambayo mwalimu anafundisha kwa kutumia visa vya kubuni au visa halisi. Njia hii inafaa sana kutumika hususan kwa watoto wadogo.
- Katika Quran njia hii imetumika kutufundisha mara kadhaa.
Kanuni na njia zenyewe katika Quran zimeelezwa katika “NJIA ZA KUFUNDISHIA KATIKA MADRASA ZETU”. Hapa ni muhtasari tu.
- Njia hii yaweza kutumika katika kufundisha Sira ya Mtume, Akhlaq, Tareikh, Fiqih hata tawhiid. Alimradi mwalimu afahamu jinsi ya kuitumia njia hiyo kwa ufanisi.
(b) Uelezeaji (Description)
- Njia hii hutumika kuelezea dhana au wazo Fulani katika uislam. Muhimu kwa mwalimu ni kuifahamu misingi ya njia hii pamoja na kuelewa mazingira yanayofaa kwa njia hii.
Mfano:
(i) Ili kutoa maf’hum(ufahamu) mzuri kuhusu “UISLAM” kama dini njia hii yafaa kutumika.
(ii) Ili kufundisha vizuri, mazingira ya vita vya Badr, Uhud, Khandaq n.k. kwa lengo la kufundisha mazingatio yanayopatikana, mwalimu aweza kutumia njia ya UELEZEAJI (Description)
- Kadhalika, cha muhimu ni maarifa kuhusu njia hii.
(c) Njia ya Uoneshaji (Demonstration)
- Ni njia inayotumika kufundishia mada zinazolenga kutoa ujuzi kwa wanafunzi kutenda matendo maalum:
Mfano:
(i) Swala ya mait.
(ii) Swala ya Faradh na Sunnah.
(iii) Kushona Sanda.
(iv) Kuosha Maiti.
(v) Kuchukua Udhu n.k.
- Mada kama hizi zikifundishwa pasipokutumia njia hizi, ueleo wa wanafunzi unaathirika.
- Mwalimu anatakiwa kuifahamu njia hii kwa madhumuni ya kuitumia kwa ufanisi.
(d) Njia ya ugunduzi na udadisi.
- Njia hii inamtaka mwalimu aoneshe tatizo kisha awaongoze wanafunzi katika kugundua suluhisho. Kwa kufanya hivi, milki ya ung’amuzi (Cognitive Facult) itakuwa imeendelezwa. Quran inasisitiza matumizi ya milki ya ung’amuzi (Cognition domain).
Mfano:
(i) Baada ya kufundisha “Tawhid” – Mwalimu anaweza kutoa habari ya kweli kuhusiana na tawhiid kisha wanafunzi wakajadili kwa mnasaba wa tawhid.
(ii) Mwalimu aweza kufundisha “Tareikh” – Hijar kutoka Makka kwenda Madina, alafu wanafunzi watatakiwa kugundua wanachojifunza.
(iii) Mwalimu anaweza kutoa tatizo liliopo katika jamii kwa mnasaba wa uislam, kisha akawataka wanafunzi waoneshe sababu na suluhisho.
(e) Njia ya Kuhifadhi.
- Hii ni muhimu sana katika elimu na maarifa ya kiislam. Mwalimu anatakiwa kuwawezesha wanafunzi kuhifadhi katika mada kadhaa.
Mfano:
(i) Katika Swala, mwalimu atumie njia rahisi kwa wanafunzi kuhifadhi.
(ii) Katika udhu, mwalimu atumie njia hii pia ili wanafunzi waweze kuhifadhi maneno muhimu.
(iii) Katika Dua, wanafunzi wahifadhishwe dua.
(iv) Katika Tarekh, wanafunzi wahifadhishwe aya na hadithi mbalimbali zinazonasibiana na matukio katika mada.
Mathalani, kufundisha Mkataba wa hudaybiya, Quran 48:1. 48:18 ni vema zikahifadhiwa.
Pia katika kufundisha AKHLAQ (Tabia) mwalimu awahifadhishe watoto, Sura ya 64.4 ikiwezekana, kulingana na umri wa watoto, Pia wahifadhi Quran 33:21.
No comments:
Post a Comment