Tuesday, 31 January 2012

MAMBO YA KUZINGATIA WAKATI WA KUJIFUNZA:

1. Jiwekee malengo ya kile unachotaka kukijua, pia jikadirie muda wa kutimiza malengo yako.
2. Wakati unapoanza kujifunza jiulize haraka haraka, Kitu gani unachokijua kuhusiana na kile unachojifunza? Kisha jiulize, wataka kujua kitu gani?
3. Ukimaliza kazi za kila somo, tafadhali rudia kile ulichojifunza kisha ieleze nafsi yako kile ulichojifunza ukiwa kama vile wamweleza mtu mwingine.
4. Jaribu kutambua baina ya masomo unayoyafahamu vizuri ukijifunza peke yako, na yale ambayo huyaelewi ukiwa peke yako.
5. Jaribu kujiwekea muda mzuri, wa kujifunza, muda ambao unakuwa makini sana, wala husinzii. Kisha utumie muda huo kwa kujifunza.
6. Jaribu kujifunza kwa muda wa dakika 30 hadi 60 kisha punzika kwa dakika 5 hadi 10 ndipo uanze tena kujifunza.
7. Ukifanikiwa kujifunza kitu na kukifahamu vizuri jipongeze pale unapopunzika kwa kufanya kitu kinachokufurahisha.

MAZINGIRA YA KUJIFUNZA.
Mazingira ya kujifunza ni kila kitu kinachomzunguka mtu anayejifunza. Ili kujifunza kwa ufanisi inatakiwa kuwepo kwa mazingira mazuri ya kujifunza, na ili kulijua hili tutazame nukta zifuatazo:
• Chagua sehemu ambayo unahisi kuwa wajisikia raha kama utajifunza ukiwa sehemu hiyo. Ni vizuri sehemu hiyo isiwe na watu wengi wanaokatisha ujifunzaji wako.
• Wakati unajifunza jaribu kuondosha vitu vyote vinavyoondoa mazingatio yako, kama vile, Tv, Redio, Kumpyuta, Dirisha lililowazi, makelele nk.
• Waeleze jamaa zako wasikusumbue wakati unapojifunza, kama hakuna jambo la msingi.
• Baadhi ya watu wanaweza kujifunza katika mazingira yasio tulivu, watu kama hawa wamebarikiwa, nao ni watu wenye sifa za kipekee kwa hiyo sio watu wa kuigwa.

KUSIKILIZA KWA UFANISI.
Kwanza kabisa tunapenda ifahamike kuwa kuna tofauti kati ya kusikia na kusikiliza. Kusika kunatokea bila kukusudia ama kusikiliza kunatokea kwa kukusudia. Kwa ibara nyingine, kusikiliza maana yake ni kuweka mazingatio katika kile unachokisikia na kujaribu kufahamu kile unachokisikiliza. Kwa faida yako, jua kuwa, kusikiliza kwa ufanisi ni elimu.
Na wataalamu wamesema kuwa: Msikilizaji mwenye ufanisi ni yule anaetoa mazingatio na mawazo yake yote kwa kile anachokisikiliza. Kwani msikilizaji mzuri ni yule anaesikiliza yanayosemwa na kuyatafakari.
Njia nzuri ya kukufanya utafakari kile unachokisikiliza ni kujiuliza maswali yanayohusiana na kile unachokisikia kisha kuyajibu kikamilifu.

Pia kuna baadhi ya wanafunzi hawapati faida inayotakiwa wakati wa kumsikiliza mwalimu na hii inatokana na sababu nyingi, miongoni mwazo ni:
1. Kutokuwa na hamu ya kusikiliza.
2. Kutojiandaa kwa ajili somo husika.
3. Kutotofautisha kati ya mambo ya msingi na yale yasiokuwa ya msingi wakati wa kusikiliza.
4. Kutokuwa na uhodari wa kusajili nukta muhimu wakati wa kusikiliza mada.

Ili kutatua matatizo haya inapasa kuzingatia yafuatayo:
1. Jiandae mapema kwa kile utakachokisikiliza.
2. Jaribu kukifanyia ufupisho na kujikumbusha kile kilichosemwa.
3. Jiulize zile nukta muhimu katika mazungmzo hayo.
4. Jaribu kumtafakari mzungmzaji ukiwa unamsikiliza.
5. Jaribu kukadiria mzungumzaji anaelekea kusema nini.
6. Jaribu kusikiliza kwa kufuatilia kile kinachoelezwa wazi wazi na mzungumzaji pia kile anachokificha.
7. Mtazame mzungumzaji wakati akizungumza, pia jaribu kuchunga harakati zake.
8. Sikiliza kile kinachosemwa kabla ya kukikosoa au kukiunga mkono. Yaani kwanza sikiliza hadi mwisho kisha unaweza kukosoa au kusifu. Kwani ukikatiza mazungumzo yake unaweza usisikie kile anachoendelea kukisema.
9. Jaribu kujizuia kongea na wasikilizaji wengine wakati mzungumzaji akiendelea kuwasilisha mada ili usiishughulishe akili na mambo yaliyo nje ya mada.
10. Andika nukta muhimu ukiwa wataka kukumbuka kile anachokisema mzungumzaji.
11. Sikiliza kwa kuzingatia ushahidi unaotolewa, na hili litakusaidia kuelewa somo husuka au hotuba nk.
12. Zingatia dhana ya msingi ya mzungumzaji wakati wa kumsikiliza.

No comments:

Post a Comment