Je, Umetanguliza Nini Akhera Ee Ndugu Muislamu?
Anasema Allaah سبحانه وتعالى :
((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَلْتَنظُرْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ لِغَدٍ وَاتَّقُوا اللَّهَ إِنَّ اللَّهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ))
((Enyi mlioamini! Mcheni Allaah, na kila nafsi iangalie inayoyatanguliza kwa ajili ya Kesho. Na mcheni Allaah, hakika Allaah Anazo khabari ya mnayoyatenda)) [Al-Hashr: 18]
Siku ya Qiyaamah katika Qur-aan imetajwa kwa majina kadhaa. Baadhi ya Maulamaa wamenukuu kwamba ni majina thelathini na moja takriban.
Miongoni mwayo; Al-Ghad (Kesho), As-Saa'ah (Saa), At-Taghaabun (siku ya hasara au Siku ya kulipizana), Yawmul-Ba'th (Siku ya kufufuliwa), Yawmul-Aakhirah (Siku ya Akhera), Yawmud-Diyn (siku ya malipo), Yawmul-Faswl (siku ya hukumu), Al-Waaqi'ah (tukio), Yawmul-Wa'iyd (siku ya makamio) na kadhalika.
عَنْ جَرِيرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ (رضي الله عنه) قَالَ: كُنَّا عِنْدَ رَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) فِي صَدْرِ النَّهَارِ فَجَاءَ قَوْمٌ عُرَاةً حُفَاةً مُتَقَلِّدِي السُّيُوفِ عَامَّتُهُمْ مِنْ مُضَرَ, بَلْ كُلُّهُمْ مِنْ مُضَرَ, فَتَغَيَّرَ وَجْهُ رَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) لِمَا رَأَى بِهِمْ مِنْ الْفَاقَةِ, فَدَخَلَ ثُمَّ خَرَجَ. فَأَمَرَ بِلاَلاً فَأَذَّنَ فَأَقَامَ الصّلاَةَ فَصَلَّى ثُمَّ خَطَبَ فَقَالَ: ((يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمْ الَّذِي خَلَقَكُمْ مِنْ نَفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالاً كَثِيرًا وَنِسَاءً, وَاتَّقُوا اللَّهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالأَرْحَامَ إِنَّ اللَّهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا)). و ((اتَّقُوا اللَّهَ وَلْتَنْظُرْ نَفْسٌ مَا قَدَّمَتْ لِغَدٍ)) ))تَصَدَّقَ رَجُلٌ مِنْ دِينَارِهِ مِنْ دِرْهَمِهِ مِنْ ثَوْبِهِ مِنْ صَاعِ بُرِّهِ مِنْ صَاعِ تَمْرِهِ وَلَوْ بِشِقِّ تَمْرَةٍ)) فَجَاءَ رَجُلٌ مِنْ الأََنْصَارِ بِصُرَّةٍ كَادَتْ كَفُّهُ تَعْجِزُ عَنْهَا, بَلْ قَدْ عَجَزَتْ, ثُمَّ تَتَابَعَ النَّاسُ حَتَّى رَأَيْتُ كَوْمَيْنِ مِنْ طَعَامٍ وَثِيَابٍ حَتَّى رَأَيْتُ وَجْهَ رَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) يَتَهَلَّلُ كَأَنَّهُ مُذْهَبَةٌ. فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم)َ: ((مَنْ سَنَّ فِي الإِِسلاَمِ سُنَّةً حَسَنَةً فَلَهُ أَجْرُهَا وَأَجْرُ مَنْ عَمِلَ بِهَا مِنْ غَيْرِ أَنْ يَنْقُصَ مِنْ أُجُورِهِمْ شَيْئًا, وَمَنْ سَنَّ فِي الإِِسلاَمِ سُنَّةً سَيِّئَةً فَعَلَيْهِ وِزْرُهَا وَوِزْرُ مَنْ عَمِلَ بِهَا مِنْ غَيْرِ أَنْ يَنْقُصَ مِنْ أَوْزَارِهِمْ شَيْئًا))
Kutoka na Jariyr bin ‘Abdullaah (رضي الله عنه) ambaye amesema :
“Tulikuwa na Mtume (صلى الله عليه وسلم) mapema mchana, wakaja watu ambao walikuwa uchi hawana viatu [walikaribia kuwa uchi kwa mavazi yao ya duni] wakiwa wemebeba mapanga yao. Wengi wao ikiwa si wote walikuwa kutoka [kabila la] Mudhwar.
Uso wa Mtume (صلى الله عليه وسلم) ukabadilika alipoona jinsi gani walivyo maskini [akawa amehuzunika].
Akaingia [nyumbani kwake] kisha akatoka nje na akamuamrisha Bilaal aadhini.
Akaswalisha watu kisha akahutubia akisema: ((Enyi watu, mcheni Allaah Ambaye Amekuumbeni kutokana na nafsi moja, kisha Akaumba kutoka humo mke wake na Akaeneza kutoka wao wawili wanaume wengi na wanawake, na mcheni Ambaye mnamuomba Kwake na jamaa zenu.
Hakika Allaah ni Mwenye kuwaangalieni)) [An-Nisaa:
1] Na ((mcheni Allaah na kila nafsi itazame imetanguliza nini kwa ajili ya kesho)) [Al-Hashr: 18] ((Atoe mtu sadaka katika dinari zake, nguo zake, ngano au tende zake hata ikiwa ni nusu ya tende moja)).
Akaja mtu kutoka Answaar akaleta furushi ambalo hakuweza hata kulibeba vizuri mkononi, kisha mwengine, kisha mwengine hadi yakawa marundi mawili ya chakula na nguo.
Nikaona uso wa Mtume (صلى الله عليه وسلم) ukinawiri kwa furaha.
Akasema Mtume (صلى الله عليه وسلم):
((Atakayeanza [kutenda] katika Uislamu kitendo chema, atapata thawabu zake na thawabu sawasawa na watakaomfuata bila ya kupunguziwa chochote katika thawabu zao.
Na atakayeanzisha [kutenda] kitendo kiovu atabeba dhambi zake na dhambi za watakaomfuata bila ya kupungiziwa katika dhambi zao chochote)) [Muslim ameisimulia Hadiyth hii kutokana na isnaad ya Shu'bah]
Hivyo jiulize Muislamu, je, umetanguliza nini Akhera? Umetimiza Swalah zako ipasavyo? Umetanguliza Swalah za Sunnah? Umetekeleza Zakaah na Sadaka? Umefunga Ramadhaani na Swawm za Sunnah? Umetekeleza Hajj na 'Umrah? Umesoma Qur-aan kwa wingi na kufuata maamrisho yake na kujiepusha na makatazo yake? Umetanguliza wema wa aina yoyote? Umeamrisha mema na kukataza maovu?
Kumbuka kwamba jema lolote utakalolitenda litakuwa ni akiba yako Aakhera na bila shaka utakuja kulikuta na utapata malipo yake siku ya Qiyaamah kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى :
((وَأَقِيمُواْ الصَّلاَةَ وَآتُواْ الزَّكَاةَ وَمَا تُقَدِّمُواْ لأَنفُسِكُم مِّنْ خَيْرٍ تَجِدُوهُ عِندَ اللّهِ إِنَّ اللّهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ))
((Na shikeni Swalah na toeni Zakah; na kheri mtakazojitangulizia nafsi zenu mtazikuta kwa Allaah, hakika Allaah Anayaona mnayoyafanya)) [Al-Baqarah: 110]
No comments:
Post a Comment